Alhamisi, 23 Juni 2016

KESSY KUIKOSA TENA TP MAZEMBE?



Shirikisho la Soka nchini (TFF) limesema litaingilia
kati kama klabu ya Simba itachelewa kujibu
maombi ya Yanga ya kumtumia beki Hassan Kessy
kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho
la Soka la Afrika (CAF-CC).
Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) liliizuia klabu ya
Yanga kumtumia beki Hassan Kessy kwenye
mchezo dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria mpaka pale
klabu yake ya zamani Simba iandike barua ya
kuiruhusu Yanga ambayo itaituma kwenye
shirikisho hilo kama uthibitisho ya kuwa hana
mkataba na klabu yake hiyo ya zamani.
Yanga iliiandikia barua klabu ya Simba juzi na
nakala ya barua hiyo kuiwasilisha TFF wakiwataka
mahasimu wao hao kutoa ruhusa kwa beki Hassan
Kessy ambaye mkataba wake na klabu yake hiyo
ya zamani unafikia kikomo Juni 30 kuichezea timu
hiyo kwenye kombe hilo.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alithibitisha
kupokea nakala ya barua hiyo ya Yanga kwenda
kwa mahasimu wao Simba juzi na kusema
wanafuatilia kama watajibiwa kwa wakati.
“Tusingeweza kuingilia kati suala hili mpaka Yanga
wenyewe waiandikie Simba kuomba ruhusa yao na
kama Simba watachelewa kuwajibu Yanga, sisi
tutaingilia kati kwa kuwapa taarifa CAF kuwa Kessy
hana mkataba na Simba na aruhusiwe kuichezea
Yanga,” alisema Lucas.
Alisema kwamba kwa kawaida mchezaji akibakiza
muda fulani wa mkataba wake anaruhusiwa
kujiunga na timu yoyote na ndivyo ilivyo kwa
Kessy, ingawa Simba wanatakiwa kutoa ushirikiano
kwa Yanga kama taratibu za CAF zinavyojieleza.
Katika hatua nyingine, TFF imesema kuwa
imepokea maombi ya Yanga ya kutaka shirikisho
hilo kuiandikia CAF wakitaka mchezo wao wa
Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika(CAF-CC)
dhidi ya TP Mazembe uchezwe Juni 29 badala ya
Juni 28.
“Yanga walipewa nafasi ya kuchagua tarehe tatu za
mchezo huo kufanyika ambapo ni tarehe 28, 29 na
30 na CAF na walitakiwa wachague moja ya tarehe
hizo na kuthibitisha CAF, lakini hawakufanya hivyo
na CAF kuamua mechi hiyo ichezwe tarehe 28 saa
10:00 jioni.
“Sasa wamekuja wakitaka tuwasaidie kuwaombea
CAF ili mchezo wao uchezwe Juni 29 saa 7:30
usiku kwa hoja ya kutoa nafasi kwa baadhi ya
mashabiki wao ambao baadhi yao ni waumini wa
dini ya Kiislamu kuweza kushuhudia mechi hiyo
na tayari tumeshawaandikia CAF na tunasubiri
majibu yao,” alisema Lucas.
Aidha, Lucas aliishutumu klabu ya Yanga kwa
kushindwa kutuma mtu kuhudhuria semina
maalumu iliyoandaliwa na CAF kwa ajili ya
mashindano hayo ambayo kwenye semina hiyo
wangepata elimu juu ya mambo mbalimbali
kuhusu ushiriki wao.
“Inashangaza sana CAF waliwatumia Yanga barua
ya mwaliko mapema sana na mwenyekiti wao
Yusuph Manji alithibitisha kuipata barua hiyo,
lakini wakaipuuza. Wangetuma mtu kwenye semina
ile ambayo CAF walikuwa wanagharamia kila kitu
wangepata elimu kubwa ya ushiriki wao kwenye
mashindano yao.
“Madhara ya kutoshiriki semina hiyo ndio kama
hayo ya kontena lao la vifaa kama vile viatu, vifaa
vya mazoezi, jezi za mechi ambazo zingetoa
nafasi ya wao kuweka nembo ndogo ya mdhamini
wao (Kilimanjaro) mabegani. Hawakuwa na jezi
hizo kwenye mchezo wa kwanza na walilazimika
kununua jezi nyingine,” alisema Lucas.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni