Jumamosi, 25 Juni 2016

TETESI ZA SOKA ULAYA JUMAPILI 26.06.2016

Meneja wa Manchester City Pep Guardiola anaamini ameshinda mbio za kumsajili beki wa Everton John Stones, 22, lakini Chelsea na Manchester United bado pia wanamfuatilia (Sun), Kiungo wa Spain na Chelsea Cesc Fabregas, 29, anasema uamuzi wa Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya utaathiri Ligi Kuu ya England (Sunday Telegraph), meneja wa Arsenal Arsene Wenger anatarajia kukutana na wawakilishi wa mshambuliaji wa Lyn, Alexandre Lacazette, 25, lakini anakabiliwa na ushindani kutoka Atletico Madrid na West Ham (Sunday Mirror), meneja wa Manchester United Jose Mourinho anaghadhibishwa na mkakati wa usajili wa Old Trafford kwa kumsajili beki mmoja tu Eric Bailly, 22, mpaka sasa (Manchester Evening News), Manchester United watalazimika kuvunja rekodi ya dunia ya pauni milioni 85.3 ambayo Real Madrid walitoa kumsajili Gareth Bale, ikiwa wanataka kumsajili kiungo wa Juventus Paul Pogba, 23 (Sunday Telegraph), Jose Mourinho ana uhakika kuwa pauni milioni 30 zitatosha kumsajili winga wa Wolfsburg Julian Draxler, 22, ikiwa atashindwa kumpata Henrikh Mhkitaryan, 27 kutoka Borussia Dortmund (Star on Sunday), Tottenham wanakabiliwa na ushindani kutoka Paris St-Germain kumsajili mshambuliaji wa AZ Almaar Vinvest Janssen, 22 (L’Equipe), Bayern Munich wamevutiwa na uchezaji wa kiungo wa Tottenham Eric Dier, 22, kwenye michuano ya Euro 2016 (Sunday People), meneja mpya wa Everton Ronald Koeman anataka kumsajili kiungo wa Manchester United Morgan Schneiderlin, 26 (Sunday Mirror), Stoke watakamilisha usajili wa mshambuliaji wa West Brom Saido Berahino, 22 wiki hii (Sunday People), Swansea wanakaribia kumsajili beki wa kari wa Ajax Mike van der Hoorn, 23, kwa mkataba wa pauni milioni 2 (Mail on Sunday), meneja wa Newcastle Rafael Benitez anajiandaa kutoa dau la pauni milioni 10 kumsajili kiungo wa Bournemouth Matt Ritchie, 26, kutokana na wasiwasi kuwa huenda Andros Townsend, 24, anaweza kuondoka (Sun).

POLANDA YAKWANZA KUTINGA ROBO FAINALI EURO 2016, SWITZERLAND YATUPWA NJE

Poland itakutana na Croatia ama Portugal katika
robo fainali ya michuano ya Euro2016 baada ya
kuishinda Switzerland kwa Penalti.
Jakub Blaszczykowski aliiweka mbele Switzerland
kabla ya Xherdan Shaqiri kusawazisha kupitia bao
zuri.
Mchezaji huyo wa Stoke alimfunga Lukas fabianski
kupitia shambulio la 'Bycycle kick' kwa lugha ya
Kiingereza.
Mchezaji aliyesajiliwa hivi majuzi na klabu ya
Arsenla Granit Xhaka alikosa penalti kwa upande
wa Switzerland baada ya mechi hiyo kuisha na
sare ya 1-1.

Alhamisi, 23 Juni 2016

VARDY AONGEZA MKATABA LEICESTER CITY.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa
wa England, Jamie Vardy
amekubali kusaini Mkataba
mpya wa miaka minne
kuendelea kuchezea klabu
yake, Leicester City na
kukataa ofa ya kujiunga na
Arsenal.
Mustakabali wa mkali huyo
wa mabao wa England
umekuwa haueleweki tangu
Arsene Wenger atangaze ofa
ya Pauni Milioni 20
kumnunua Juni 3, mwaka
huu, lakini ameipiga chini ofa
hiyo na kuamua kubaki
Uwanja wa King Power.
Baada ya Arsenal kumpa ya
mshahara wa Pauni 120,000
kwa wiki, Leicester City nayo
imemuongezea mshahara
mchezaji huyo hadi pauni
100,000 kwa wiki na Vardy
atasaini Mkataba mpya
atakaporejea kutoka kwenye
Euro 2016 nchini Ufaransa.
Vardy aliisaidia Leicester City
kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu
ya England akifunga jumla ya
mabao 24 msimu uliopita
Mbali ya mshahara mkubwa
zaidi, lakini Vardy
angenufaika zaidi kwa kipato
Uwanja wa Emirates kutokana
na hali nzuri ya kiuchumi na
sera za malipo za Arsenal
ukilinganisha na Leicester.
Iwapo atasaini Mkataba
mpya, mchezaji huyo
mwenye umri wa miaka 29
atadumu King Power hadi
mwaka 2020 atakapofikisha
umri wa miaka 33 – jambo
ambalo ni habari njema kwa
kila mmoja ndani ya
Leicester City.
Vardy alikuwa chachu ya
mafanikio ya Leicester City
msimu uliopita ikitwaa
ubingwa wa Ligi Kuu ya
England, akifunga jumla ya
mabao 24.

SALUM KIMENYA ATAKA MIONI 40 KUMWAGA WINO MSIMBAZI

Beki wa kati wa Tanzania Prisons, Salum Kimenya,
amesema anahitaji Sh milioni 40 ili aweze
kumwaga wino kwenye kikosi cha Wekundu wa
Msimbazi, Simba, kwa mujibu wa Mtanzania.
Kimenya ambaye amekuwa kwenye kipindi cha
mafanikio msimu uliopita, amesema hakuna
kinachomkwamisha kutua kwenye klabu hiyo zaidi
ya fedha anayoitaka.
Alisema dau dogo ambalo amekuwa akitajiwa na
viongozi hao wa Simba, ndilo limekuwa kikwazo
cha yeye kutua kwenye klabu hiyo.
“Simba mwaka jana walinitaka wakataka kunipa
milioni 30 nikakataa nikawaambia nipeni 45 dili
likavunjika na safari hii nawashangaa kabisa dau
lao eti wanataka kunipa Sh milioni 20,
nimewaambia wanipe 50 pia imekuwa ni kuomba
wapunguziwe sasa imefika 40 hapo siwezi
kupunguza tena,” alisema.
Kimenya alisema amewapa muda viongozi hao wa
Simba mwisho wiki hii, ikifika Jumatatu ijayo basi
atatia saini kwenye klabu yake ya Prisons.
“Nawapa mpaka wiki hii iwe mwisho kama
wakikaa kimya basi nitasajili kwenye klabu yangu
ya Prisons ambayo nimemaliza nayo mkataba,”
alisema.
Simba inasuka upya kikosi chake msimu ujao
ambapo mpaka sasa tayari imewasajili nyota
watano ambao ni mabeki; Emmanuel Semwanza,
kiungo Muzamil Yasir, Mohammed Ibrahim, Hamad
Juma na mshambuliaji, Jamal Mnyate.

KESSY KUIKOSA TENA TP MAZEMBE?



Shirikisho la Soka nchini (TFF) limesema litaingilia
kati kama klabu ya Simba itachelewa kujibu
maombi ya Yanga ya kumtumia beki Hassan Kessy
kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho
la Soka la Afrika (CAF-CC).
Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) liliizuia klabu ya
Yanga kumtumia beki Hassan Kessy kwenye
mchezo dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria mpaka pale
klabu yake ya zamani Simba iandike barua ya
kuiruhusu Yanga ambayo itaituma kwenye
shirikisho hilo kama uthibitisho ya kuwa hana
mkataba na klabu yake hiyo ya zamani.
Yanga iliiandikia barua klabu ya Simba juzi na
nakala ya barua hiyo kuiwasilisha TFF wakiwataka
mahasimu wao hao kutoa ruhusa kwa beki Hassan
Kessy ambaye mkataba wake na klabu yake hiyo
ya zamani unafikia kikomo Juni 30 kuichezea timu
hiyo kwenye kombe hilo.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alithibitisha
kupokea nakala ya barua hiyo ya Yanga kwenda
kwa mahasimu wao Simba juzi na kusema
wanafuatilia kama watajibiwa kwa wakati.
“Tusingeweza kuingilia kati suala hili mpaka Yanga
wenyewe waiandikie Simba kuomba ruhusa yao na
kama Simba watachelewa kuwajibu Yanga, sisi
tutaingilia kati kwa kuwapa taarifa CAF kuwa Kessy
hana mkataba na Simba na aruhusiwe kuichezea
Yanga,” alisema Lucas.
Alisema kwamba kwa kawaida mchezaji akibakiza
muda fulani wa mkataba wake anaruhusiwa
kujiunga na timu yoyote na ndivyo ilivyo kwa
Kessy, ingawa Simba wanatakiwa kutoa ushirikiano
kwa Yanga kama taratibu za CAF zinavyojieleza.
Katika hatua nyingine, TFF imesema kuwa
imepokea maombi ya Yanga ya kutaka shirikisho
hilo kuiandikia CAF wakitaka mchezo wao wa
Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika(CAF-CC)
dhidi ya TP Mazembe uchezwe Juni 29 badala ya
Juni 28.
“Yanga walipewa nafasi ya kuchagua tarehe tatu za
mchezo huo kufanyika ambapo ni tarehe 28, 29 na
30 na CAF na walitakiwa wachague moja ya tarehe
hizo na kuthibitisha CAF, lakini hawakufanya hivyo
na CAF kuamua mechi hiyo ichezwe tarehe 28 saa
10:00 jioni.
“Sasa wamekuja wakitaka tuwasaidie kuwaombea
CAF ili mchezo wao uchezwe Juni 29 saa 7:30
usiku kwa hoja ya kutoa nafasi kwa baadhi ya
mashabiki wao ambao baadhi yao ni waumini wa
dini ya Kiislamu kuweza kushuhudia mechi hiyo
na tayari tumeshawaandikia CAF na tunasubiri
majibu yao,” alisema Lucas.
Aidha, Lucas aliishutumu klabu ya Yanga kwa
kushindwa kutuma mtu kuhudhuria semina
maalumu iliyoandaliwa na CAF kwa ajili ya
mashindano hayo ambayo kwenye semina hiyo
wangepata elimu juu ya mambo mbalimbali
kuhusu ushiriki wao.
“Inashangaza sana CAF waliwatumia Yanga barua
ya mwaliko mapema sana na mwenyekiti wao
Yusuph Manji alithibitisha kuipata barua hiyo,
lakini wakaipuuza. Wangetuma mtu kwenye semina
ile ambayo CAF walikuwa wanagharamia kila kitu
wangepata elimu kubwa ya ushiriki wao kwenye
mashindano yao.
“Madhara ya kutoshiriki semina hiyo ndio kama
hayo ya kontena lao la vifaa kama vile viatu, vifaa
vya mazoezi, jezi za mechi ambazo zingetoa
nafasi ya wao kuweka nembo ndogo ya mdhamini
wao (Kilimanjaro) mabegani. Hawakuwa na jezi
hizo kwenye mchezo wa kwanza na walilazimika
kununua jezi nyingine,” alisema Lucas.